25 Mei 2025 - 23:11
Source: Parstoday
Waandamanaji Ulaya wataka jamii ya kimataifa izuie Israel kuendeleza mauaji ya kimbari Gaza

Maelfu ya waandamanaji mjini Berlin, Paris na Stockholm wametaka serikali zao zivunje ukimya kuhusu vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na Israel huko Gaza, wakihimiza hatua ya haraka ya kimataifa na vikwazo dhidi ya utawala huo.

Huko Berlin, maelfu ya watu walikusanyika katika eneo la Oranienplatz siku ya Jumamosi kupinga mashambulizi makali ya anga na uvamizi wa ardhini unaofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza. Waandamanaji walipaza sauti wakisema: “Uhuru kwa Palestina,” “Ujerumani inafadhili, Israel inabomoa,” “Israel ni dola la kigaidi,” na “Sitisha mauaji ya kimbari.”

Waandamanaji wa Kijerumani wamesema kuwa hakuna mtu wala taifa lolote lenye haki ya kuwanyima watu haki zao, kuwafurusha makwao, au kuwafanyia vitendo vya kikatili. Baadhi ya waandamanaji wa Kiyahudi pia walishiriki kwenye maandamano hayo.

Mjini Paris, watetezi wa haki za Wapalestina wamekusanyika katika uwanja wa Bourse, wakitoa wito wa kuwekwa vikwazo dhidi ya Israel na kuruhusiwa misaada ya kibinadamu kuingia Gaza bila vizuizi. Waandamanaji wa Paris walionesha hali mbaya ya njaa inayokumba Gaza kutokana na mzingiro uliowekwa na Israel kwa kugonga sufuria na vyombo vitupu huku wakipaza sauti: “Israel ni muuaji, Macron ni mshirika,” na “Kuna mauaji ya kimbari Gaza; hatutakaa kimya.”

Myriem, mwanamke mwenye umri wa miaka 44, aliviambia vyombo vya habari kuwa alihudhuria maandamano hayo kupinga uungaji mkono wa serikali ya Ufaransa kwa Israel na kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina wanaoteseka. Ameeleza vizuizi dhidi ya misaada ya kibinadamu kwa Gaza kuwa ni “unyama” na “fedheha,” na akatoa wito wa kuhamasisha umma haraka.

Katika mji wa Stockholm, mamia ya watu walikusanyika katika uwanja wa Odenplan kufuatia mwito kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kiraia, wakiitaka serikali ya Uswidi kuchukua hatua dhidi ya uhalifu wa kivita unaoendelea kufanywa na Israel huko Gaza. Waandamanaji walitembea hadi Wizara ya Mambo ya Nje ya Uswidi, wakiimba: “Uhuru kwa Palestina,” na “Hapana kwa mpango wa Netanyahu.”

Tangu tarehe 2 Machi, hali ya kibinadamu Gaza imezidi kuwa mbaya sana kutokana na vizuizi vikali vya utawala wa Israel dhidi ya kuingizwa chakula, mafuta, dawa na maji katika eneo hilo. Hiki ni kipindi kirefu zaidi cha mzingiro kamili wa Gaza tangu vita kuanza tarehe 7 Oktoba 2023.

Kwa mujibu wa Mpango wa Pamoja wa Usalama wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (IPC), Gaza iko katika awamu ya tano ya njaa kali, ambapo takribani watoto 71,000 walio chini ya miaka mitano wako katika hatari ya utapiamlo mkali. IPC huelezea awamu ya tano kuwa ni hali ambapo angalau familia moja kati ya tano inakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula na inakabiliwa na hatari ya njaa kali, umasikini wa kupindukia, viwango vya juu vya utapiamlo mkali na vifo.

Your Comment

You are replying to: .
captcha